Alhamisi, 01 Novemba 2012 15:37
>>IFUATAYO NI TAARIFA KAMILI YA TFF:
TANZANIA FOOTBALL FEDERATION (TFF)
ELECTIONS COMMITTEE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UAMUZI KUHUSU RUFANI DHIDI YA
KAMATI ZA UCHAGUZI ZA VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU MKOA WA MWANZA (MZFA),
MKOA WA GEITA (GEREFA) NA KUHUSU MICHAKATO YA UCHAGUZI YA VYAMA
WANACHAMA WA TFF NA WANACHAMA WAO
OKTOBA 31, 2012
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia
Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF
Ibara ya 8(2), 10(6), 12(1) na 26(2) na (3) katika kikao chake
kilichofanyika Oktoba 30, 2012 ilijadili rufani dhidi ya Kamati za
Uchaguzi za MZFA na GEREFA na michakato ya uchaguzi ya vyama vya mpira
wa miguu vya mikoa ya Mwanza, Rukwa, Chama cha Mpira wa Miguu wa
Wanawake (TWFA), Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) na
Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na kutoa uamuzi kama ifuatavyo;
1. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)
(a) Rufani ya Ndg. Jackson Manji Songora: Kamati
ilijadili rufani iliyowasilishwa na Ndg. Jackson Manji Songora dhidi ya
Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF
kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kumpitisha Ndg. Jumbe
O. Magati kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MZFA, kwamba Kamati ya
Uchaguzi ya MZFA ilikosea:
(i)Kupokea Statement of Results ya
Baraza la Mitihani Tanzania yenye jina la Fredrick J. Magati wakati
jina la mgombea alilojaza kwenye fomu ya maombi ya uongozi ni Jumbe O.
Magati.
(ii)Kumsaili Jumbe O. Magati kwa kuwa hakuwasilisha nakala halisi ya cheti cha elimu yake.
(iii)Kumpitisha Ndg. Jumbe O. Magati
kugombea uongozi na kuwa Ndg. Jumbe O. Magati hana sifa zinazokidhi
matakwa ya Katiba ya MZFA Ibara ya 29(2).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia
maelezo ya Mrufani na ilijiridhisha kuwa rufani iliyowasilishwa mbele
yake na Ndg. Songora haikutanguliwa na pingamizi mbele ya Kamati ya
Uchaguzi ya MZFA, hivyo ilikosa sifa ya kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni
za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya
TFF Ibara ya 49(1); Katiba ya MZFA Ibara ya 47 na Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF Ibara ya 26(2), Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa kutumia
mamlaka yake ya kikatiba na kanuni za uchaguzi, ilimuhoji Ndg. Magati
kuhusu elimu yake na majina yaliyo kwenye Statement of Results na fomu yake ya maombi ya uongozi.
Baada ya kupitia vielelezo na maelezo
yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu majina ya Ndg. Jumbe O. Magati,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa Jumbe O. Magati na Fredrick
J. Magati ni mtu huyo huyo. Kamati ya Uchaguzi imetupa rufani ya Ndg. Patrick Manji Songora.
2. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA)
(a) Rufani ya Ndg. Abdallah H. Hussein: Kamati
ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Abdallah H. Hussein
ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake
kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha
kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Geita. Kamati ilipitia vielelezo
vilivyowasilishwa mbele yake na Mrufani na ilijiridhisha kuwa vielelezo
hivyo vinakidhi kuthibitisha kuwa mwombaji uongozi ni Mkazi wa Mkoa wa
Geita. Kamati inakubaliana na maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg.
Abdallah H. Hussein kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
(b) Rufani ya Ndg. Aziz Mwamcholi: Kamati
ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Aziz Mwamcholi
ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake
kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa GEREFA, kwa kigezo cha kushindwa
kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari. Kamati ilipitia maelezo ya
Ndg. Mwamcholi na ya Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA na ikajiridhisha kuwa
Ndg. Mwamcholi hakukidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa
TFF, hususan Ibara ya 10(5). Kamati imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi ya GEREFA wa kutompitisha Ndg. Mwamcholi kugombea nafasi ya
Makamu Mwenyekiti wa GEREFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetupa rufani hiyo.
(c) Rufani ya Ndg. Kaliro Samson: Ndg.
Samson aliwasilisha rufani kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya
GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
TFF kwa kigezo cha kutowasilisha cheti cha kuhitimu elimu ya kidato cha
nne. Kamati ilipitia maelezo na vielelezo vya rufani ya Ndg. Samson nay a
Mrufaniwa na kujiridhisha kuwa nakala ya cheti cha elimu ya kidato cha
sita inakidhi matakwa ya Katiba ya GEREFA Ibara ya 29(2). Kamati
inakubaliana na maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg. Kaliro Samson
kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
3. Mchakato wa Uchaguzi Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili
mchakato wa uchaguzi wa MZFA ikiwa ni pamoja na mchakato wa uchaguzi wa
Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ukerewe (UDFA), baada ya uchaguzi wa
awali wa UDFA kuwa umefutwa na Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kutokana na
Kamati ya Uchaguzi ya UDFA kutozingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama
wa TFF.
Baada ya maelezo ya kina ya Kamati ya
Uchaguzi ya MZFA na vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu
mwenendo wa uchaguzi wa UDFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa
kuna ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu za uchaguzi uliofanywa na
Kamati ya Utendaji ya UDFA kwa kutozingatia kikamilifu maagizo ya Kamati
ya Uchaguzi ya MZFA na hivyo kusababisha mkanganyiko katika mchakato wa
Uchaguzi ambao kwa wakati mmoja ulikuwa na Kamati mbili za Uchaguzi
kusimamia uchaguzi huo. Mikanganyiko inayojionyesha dhahiri na
kusababisha nafasi zote sita zinazogombewa katika mchakato unaoendelea
kuwa na mgombea mmoja mmoja tu katika kila nafasi, imeufanya mchakato wa
uchaguzi wa UDFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za
Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa katika
Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka yake ya
kikatiba Ibara ya 49(1) ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF, Ibara ya 10(6) na 26(2) na (3) imeamua:
(i)Kuzifuta Kamati zote za Uchaguzi za
UDFA zilizoteuliwa na Kamati ya Utendaji ya UDFA kabla ya baada ya
mchakato wa uchaguzi wa sasa wa UDFA.
(ii) Kuufuta Uchaguzi wa UDFA uliokuwa
ufanyike Novemba 5, 2012. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya kwa tarehe
zitakazopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya MZFA baada ya kupata maelekezo
ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
(iii) Kuiagiza Kamati ya Uchaguzi ya
MZFA katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Ibara ya 6 ya Kanuni
za Uchaguzi za Wanachama wa TFF kutoiruhusu UDFA kushiriki Mkutano Mkuu
wa Uchaguzi wa MZFA kwa kuwa UDFA imeshindwa kuzingatia matakwa ya
Katiba kuhusu ukomo wa mamlaka ya Kamati ya Utendaji na kufanya uchaguzi
kwa wakati muafaka unaozingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
4. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA)
Kwa kuzingatia changamoto za kuijenga
TWFA ambayo bado ni change, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekubali ombi la
TWFA la kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi kwa wiki mbili. Uchaguzi wa
TWFA ngazi ya Taifa sasa utafanyika Novemba 18, 2012.
5. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)
Uchaguzi wa viongozi wa FRAT utafanyika Novemba 17, 2012 kama ulivyopangwa.
6. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)
TFF imesimamisha kuanza kwa mchakato wa
uchaguzi wa RUREFA kutokana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya RUREFA
kuendeleza malumbano kati yao kuhusu uhalali wa uteuzi wa Kamati mpya ya
Uchaguzi ya RUREFA, uteuzi ambao ulifanywa na Kamati ya Utendaji ya
RUREFA, Oktoba 18, 2012. Kwa kuwa hali hii imetokea tena baada ya Kamati
ya Utendaji ya RUREFA kuwa imepewa fursa ya kikatiba
kuteua Kamati ya Uchaguzi na ni mwendelezo wa mgawanyiko ndani ya Kamati
ya Utendaji ya RUREFA unaoathiri mchakato wa uchaguzi wa chama hicho,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatafakari hatua muafaka za kikatiba na
kikanuni zitakazoondoa ukwamishaji wa mchakato wa Uchaguzi wa RUREFA
unaosababishwa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA. Uamuzi kuhusu
mustakabali wa Uchaguzi wa RUREFA utatolewa baada ya kikao cha Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Novemba 6, 2012.
7. Mchakato wa Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na Chama cha Makocha (TAFCA)
Uamuzi kuhusu mustakabali wa uchaguzi wa
SPUTANZA na TAFCA utatolewa baada ya vyama hivyo kuwasilisha taarifa za
kina kuhusu michakato ya chaguzi za wanachama wao katika ngazi ya
mikoa, katika kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika
Novemba 6, 2012.
Moses Kaluwa
Mjumbe- Kamati ya Uchaguzi TFF



No comments:
Post a Comment