![]() |
Mbuyu Tweite aka Rage |
USAJILI wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu umekuwa na msisimko wa aina yake, kutokana na ‘umafia’ waliofanyiana watani wa jadi, Simba na Yanga- jambo ambalo limekumbushia baadhi ya matukio ya aina hiyo miaka iliyopita, kama lile la Victor Costa kusaini Yanga na kujiunga nao, kisha kurejea Simba na kuvaa jezi yenye jina la aliyempa fedha kusaini fomu Jangwani, Jamal Malinzi, aliyekuwa Katibu wa Yanga wakati huo. Safari hii, Mbuyu Twite alipewa dola za Kimarekani 30,000 na Ismail Aden Rage, Mwenyekiti wa Simba na kusaini, lakini akasaini pia na kuhamia Yanga kutoka APR na alipofika Dar es Salaam akavaa jezi yenye jina la Mtanzania huyo mwenye asili ya Kisomali. DIMBANI LEOinakukumbusha baadhi ya vituko hivyo na kuamua kukipa ‘namba moja’ kituo cha Rage.
YUSSUF ISMAIL BANA
![]() |
Yussuf Bana kushoto akiichezea Yanga dhiai ya Simba. Kulia ni Zamoyoni Mogella na nyuma ni Muhiddin Cheupe. |
AKIWA mchezaji wa Pamba ya Mwanza mwanzoni mwa miaka ya 1980, beki Yussuf Ismail Bana alisaini Simba katika fomu za usajili akitumia jina la Yussuf Ismail. Lakini baadaye Yanga wakamfuata na kumrubuni asaini kwao. Akasaini Jangwani na kutumia jina la Yussuf Bana na Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF) chini ya Mwenyekiti wake wa enzi hizo, Said Hamad El Maamry wakamuidhinisha kuchezea Yanga, lilikuwa bonge la sinema.
CHARLES BONIFACE MKWASA
Charles Boniface Mkwasa |
Akiwa mchezaji mpya kwenye kikosi cha Yanga aliyesajiliwa kutoka Tumbaku ya Morogoro, mwanzoni mwa miaka ya 1980, Simba ilimfuata na kumrubuni ahamie kwao. Kiungo Charles Boniface Mkwasa, akakubali na kusaini Simba SC kwa jina la Charles Boniface alilokuwa pia akitumia Yanga na tangu Tumbaku. Lakini Yanga wakamfuata na kumshawishi abaki, na baada ya kukubaliana naye, akasaini kuendelea kuichezea Yanga, safari hii akitumia jina la Charles Boniface Mkwasa. Lakini hii mbele ya FAT ya El Maamry ilidunda na Mkwasa alifungiwa msimu mzima kabla ya kumaliza adhabu yake na kuendelea kucheza Jangwani.
EPHRAIM MAKOYE MAHALA:
Akiwa mchezaji mpya kwenye kikosi cha Yanga aliyesajiliwa kutoka Kagera Stars mwaka 2000 (sasa Kagera Sugar), Simba SC walimfuata na kumrubuni asaini kwao. Makoye, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika sekondari ya Makongo, alichukua fedha za Simba akasiani. Hata hivyo, siku hiyo hiyo Yanga walimnasa na kumchukua hadi kwa viongozi wa Simba kurudisha fedha alizochukua aendelee kuchezea Yanga. Simba waligoma kuchukua fedha na kwa sababu wakati huo FAT ilikuwa haitambui mikataba ya klabu na mchezaji zaidi ya fomu za usajili, ambazo zilikuwa hazijatoka, Makoye aliendelea kuchezea Yanga, ingawa baadaye alichezea Simba alipotemwa Yanga.
VICTOR COSTA
![]() |
Victor Costa aka Malinzi |
Akiwa mchezaji mpya aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar kwenye kikosi cha Simba mwaka 2005, Yanga walimfuata beki huyo na kumrubuni asaini kwao. Costa alisaini na kwenda kujiunga na wenzake kambini Zanzibar ambako timu ilikuwa inacheza Kombe la Mapinduzi. Lakini aliporejea tu Dar es Salaam, Simba wakamteka na kumpeleka mazoezini kwao, akiwa amevaa jezi iliyoandikwa jina la Katibu Mkuu wa Yanga wakati huo, Jamal Malinzi. Costa hakurudisha fedha za Yanga na akaidhinishwa kuendelea kuchezea timu yake.
MBUYU TWITE:
Akiwa amekwishasaini mkataba wa kuichezea Simba SC kutoka APR ya Rwanda, Yanga wakamzungukia na kumsainisha na beki huyo akaamua kurudisha fedha za Simba. Tukio hilo lilimtoa machozi Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dodoma kulaani kitendo hicho. Tukio hilo siyo tu linapanda kileleni katika vituko vya usajili wa Ligi Kuu ya Bara kwa sababu ndilo la sasa, bali pia kwa kitendo cha ‘mtu mzima’ Rage kumwaga machozi mbele ya kamera za Televisheni akisikitikia changa la macho alilopigwa na mchezaji huyo.
![]() |
Rage akilia huku akiwa amekumbatiwa vizuri na kubembelezwa na Profesa Philemon Sarungi. Hapa ilikuwa kwenye msiba wa Patrick Mafisango. |
No comments:
Post a Comment