Friday, September 7, 2012

SIMBA ONDOENI SHAKA, AKUFFO YUKO SHWARI


Akuffo katika mechi ya jana

HALI ya mshambuliaji wa Simba SC, Daniel Akuffo ni njema na leo anaweza kuendeleza na mazoezi na wenzake kwenye Uwanja wa Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Akuffo aliumia jana katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Sofapaka ya Kenya, ambao Simba SC walifungwa kwa mabao 3-0.
Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ameiambia  jana kwamba, Akuffo alipata mshituko mkubwa kwa kuchezewa rafu mbaya ghafla kiasi cha ulimi kugeuka na kupoteza fahamu, lakini baada ya jitihada za haraka, alipona.
“Jitihada za haraka za kumpatia tiba makini ya huduma ya kwanza zilisaidia, yuko sawasawa na hana tatizo lolote, alipoteza fahamu, lakini tulipofanikiwa kuurejesha ulimi katika hali ya kawaida, ilikuwa mwisho wa tatizo,”alisema Kapinga.
Daktari huyo wa mabingwa wa Tanzania Bara, alisema kwamba klabu hiyo haina majeruhi zaidi na wachezaji wanaokosekana kwa sasa ni washambuliaji Mzambia Felix Sunzu ambaye kwenye mazishi ya dada yake na Emmanuel Okwi ambaye yupo na timu ya taifa ya kwao, Uganda.  
Simba jana ilishindwa kuwafurahisha mashabiki wake Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kufungwa mabao 3-0 na Sofapaka ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumanne ijayo kwenye Uwanja huo huo.
Hadi mapumziko, Sofapaka walikuwa kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, John Barasa kwa penalti dakika ya 19, akiupeleka mpira kulia na Juma Kaseja akichupa kushoto upande wa kushoto.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya Komabil Keita kuunawa mpira kwenye eneo la hatari wakati akiwa katika jitihada za kuokoa hatari langoni mwake.
Kipindi cha pili, Sofapaka walirudi na moto tena na kufanikiwa bao la pili dakika ya 55 mfungaji Barasa tena kabla ya Joseph Nyaga kufunga la tatu dakika ya 66.
Mechi ya jana ilikuwa ya kwanza kwa Akuffo tangu ajiunge na Simba anashindwq kuifungia bao timu yake hiyo mpya na hiyo unaweza kusema kwa sababu alicheza dakika 40 tu kabla ya kuumia.
Awali, Akuffo aliifungia Simba katika kila mechi, kwenye tatu za kirafiki ilizocheza ikiwa kambini Arusha, dhidi ya Mathare United, (2-1), JKT Oljoro (2-1) na Sony Sugar (1-1).   
Simba inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Azam FC, ambayo kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kukutanisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 
MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka          Mshindi   Matokeo
2001               Yanga       2-1 Simba
2010               Yanga       0-0 Simba (3-1penalti)
2011               Simba       2-0 Yanga

No comments:

Post a Comment