Friday, November 2, 2012

SIMBA WAJICHIMBIA USAMBARA KUISUBIRI MTIBWA JUMAPILI


Wachezaji wa Simba

Na zainabu kilimu
SIMBA SC imeendelea kubaki mkoani Morogoro, baada ya sare ya 1-1 na Polisi juzi, kujiandaa na mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo.
Simba imeweka kambi Usambara Hotel, maeneo ya Nane Nane mkoani humo, huku ikijifua kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Wekundu hao wa Msimbazi, wamepania kushinda mechi ya kwanza nje ya Dar es Salaam, baada ya awali kutoa sare katika mechi zake zote za ugenini.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba ilitoka sare za bila kufungana na wenyeji Coastal Union na Mgambo JKT kabla ya juzi kufungana 1-1 na Polisi, tena yenyewe ndio ikihaha hadi kipindi cha pili kukomboa bao, baada ya Mokili Rambo kutangulia kuwafungia Maafande hao kipindi cha kwanza.
Mkombozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, alikuwa ni kiungo Amri Kiemba juzi, ambaye hilo linakuwa bao lake la nne msimu huu.
Pamoja na hayo, Simba inajivunia kuwa timu pekee ambayo hadi sasa haijapoteza mechi hata moja katika Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 23 sawa na Yanga, baada ya kucheza mechi 11, lakini ina wastani mzuri zaidi wa mabao.
Zaidi ya sare hizo tatu, Simba ilitoa sare nyingine mbili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba 2-2 na Yanga SC, wapinzani wao wa jadi, 1-1.

No comments:

Post a Comment