Jumanne, 04 Septemba 2012 20:11

Zifuatazo ni habari fupi fupi za Soka ambazo zinahusu Kiungo wa Tottenham, Tom Huddlestone, kufutiwa Kadi Nyekundu, Straika wa zamani wa Manchester United Michael Owen kujiunga na Stoke, Chelsea kumuacha Florent Malouda kwenye Kikosi chake cha Ulaya na Kiungo wa Real Madrid Lassana Diarra kuhamia to Anzhi Makhachkala.
Tom Huddlestone afutiwa Nyekundu!
Kiungo wa Tottenham Hotspur Tom Huddlestone amefutiwa Kadi Nyekundu aliyopewa kwenye Mechi ya Ligi Kuu England walipotoka sare 1-1 na Norwich City Uwanja wa White Hart Lane Jumamosi iliyopita.
Huddlestone, ambae aliingizwa toka Benchi Kipindi cha Pili ili kucheza Mechi yake ya kwanza kwa zaidi ya Mwaka baada ya kuwa majeruhi, alipewa Kadi Nyekundu na Refa Mark Halsey katika Dakika ya 90 kwa rafu kwa Jonny Howson, rafu ambayo marudio yake kwenye TV yalionyesha haikustahili Kadi yeyote.
Tottenham walikata Rufaa kupinga Kadi Nyekundu na wameshinda hivyo Mchezaji huyo yuko huru kucheza Mechi yao inayofuata hapo Septemba 16 ugenini na Reading.
Michael Owen
Zipo taarifa thabiti kuwa Michael Owen ametua Stoke City ili kukamilisha usajili wake kwa Mkataba wa Miaka miwili ambao unaaminika utakuwa na kipengele cha yeye kulipwa tu ikiwa atacheza Mechi kutokana na historia yake ya kuumia mara kwa mara.
Owen, Miaka 32, yuko huru kujiunga na Klabu yeyote hivi sasa kwa vile Klabu yake Manchester United imemuacha hivyo hazuiwi kujiunga na Klabu nyingine licha ya Dirisha la Uhamisho kufungwa Agosti 31.
Malouda atemwa Ulaya!
Chelsea imemuacha Florent Malouda katika Kikosi chao cha Wachezaji 22 ambao wamesajiliwa UEFA kucheza hatua ya Makundi ya CHAMPIONZ LIGI.
Tangu Msimu huu uanze, Malouda, Miaka 32, amekuwa hayumo kwenye Kikosi chochote cha Mabingwa wa Ulaya Chelsea ambacho kimekuwa kikicheza Mechi za Ligi Kuu England.
Hivi karibuni Chelsea imekuwa ikiwatoa Wachezaji wake ambao ni pamoja na Raul Meireles aliejiunga na Fenerbahce Jumatatu na Michael Essien aliehamia kwa mkopo Real Madrid Ijumaa iliyopita.
Pamoja na Malouda, Kipa veterani Hilario nae hayumo kwenye Kikosi hicho cha UEFA.
Diarra yupo Urusi!
Kiungo wa Real Madrid Lassana Diarra amekamilisha Uhamisho wake kwa Mabingwa wa Urusi Anzhi Makhachkala kwa kusaini Mkataba wa Miaka minne.
Mapema juzi Real Madrid ilitangaza Diarra atahamia Anzhi Makhachkala mkopo wa Msimu mmoja lakini sasa hilo limebadilika baada ya yeye kusaini Mkataba wa kudumu.
Huko Anzhi Makhachkala, Diarra anaungana na Majina maarufu wakiwemo Samuel Eto'o, Christopher Samba na Yuri Zhirkov.
Diarra alijiunga na Real Madrid Januari Mwaka 2009 akitokea Portsmouth.
No comments:
Post a Comment