Friday, September 7, 2012

KIBOKO YA SIMBA ASEMA; NINGEBAKI YANGA SIJUI KAMA NINGEKUWA NACHEZA HADI LEO


John Barasa jana


JOHN Barasa, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, amesema hana uhakika kama angebaki Yanga mwaka 2006 angekuwa hadi leo anacheza soka na hawezi kusema chochote kwa sababu soka ya Afrika Mashariki inafanana.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Barasa ambaye aliifungia Sofapaka mabao mawili katika ushindi wa 3-0 ndhidi ya Simba jana, alisema soka ni biashara nzuri, lakini si kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Barasa alisema umefika wakati viongozi wa soka wa ukanda huu wabadilike ili soka iwaingizie fedha wachezaji waifurahie na klabu ziingize fedha kwa kuendeshwa kibiashara.
“Unaona zile timu za England, usidhani kwamba hata zikija hapa Tanzania zinaweza kuzifunga Simba na Yanga, lakini soka ni furaha kwao, kwa sababu wanalipwa vizuri wachezaji na klabu zinafanya biashara ya fedha nyingi,”alisema Barasa.
Lakini pia Barasa alisema siri ya mafanikio yake, kucheza muda mrefu tena kwa kiwango cha juu ni kutokana na kujitunza na kuacha anasa. “Najitunza, mazoezi, na ninaachana na mambo mengine,”alisema Barasa.
Huyo ni mshambuliaji ambaye alitupiwa virago Yanga baada ya msimu wa 2005, akiitwa mzee. Barasa alipoondoka Yanga, akaiachia klabu hiyo mchezaji mwingine, Maurice Sunguti, ambaye naye alitemwa mwaka 2008 pia akiitwa mzee.
Beki wa kati, Paschal OIchieng aliyesajiliwa na Simba msimu huu kutoka AFC Leopard ya Kenya, alicheza na Barasa katika klabu ya Yanga mwaka 2005.

No comments:

Post a Comment